TUKIWALINDA WATOTO WANAOISHI MITAANI TUMELINDA TAIFA LA KESHO.(NAWATAKIA SIKU NJEMA YA MTOTO WA AFRIKA )
BARUA KWA MHARIRI
Mpendwa mhariri,
Je ni kweli mitaa huzaa watoto!?, jibu ni kwamba hakuna mtoto alie zaliwa na mtaa, sasa inakuaje tunawaita watoto wa mtaani!?
- Leo ninaandika barua hii nikiwa na huzuni kubwa sana moyoni baada ya kuwaona watoto katika barabara wakizunguka na kuomba omba bila ya mafanikio.
- Kula kwao ni kwa taabu sana kwani hawawezi kufanya kazi ili kujipatia mkate wao wa kila siku kutokana na umri mdogo walio nao hivyo husababisha wao kuomba omba barabarani bila kuambulia chochote zaidi ya matusi na fedheha kutoka kwa watu wazima.
- Mpendwa mhariri watoto hao mavazi na makazi kwao ni mzigo mzito wa misumari vichwani mwao, mavazi yao ni duni saana na kila linapoingia giza hujikusanya na kulala katika mavaranda ya majengo ama wengine hulala mitaroni , baridi, mbu na bugudha zote za giza huwakumba watoto hawa ambao ni watoto wetu lakini tumeamua kuukabidhi mtaa na kuwaita watoto wa mtaani.
- Tunasema ni lazima kupigana na adui ujinga na serikali inatoa elimu bure lakini watoto hawa hawapati elimu, je ni kweli adui huyu "ujinga" tutamshinda?
- Mbali na changamoto zote hizo wanazokutana nazo bado kuna baadhi ya watu wazima huwafanyia matendo ya kinyama kama kuwaingilia kingono (wa kike kubakwa na wa kiume kulawitiwa) daah tumekosa ubinaadamu kabisa .Watu wazima huyafanya haya yote ili tu kukata kiu ya tamaa za miili yao.
Ningepanda kuwaomba ndugu zangu, mashirika binafsi na serikali kiujumla kulitazama swala hili kwa jicho la tatu, naamini sote tukishikamana tunaweza kuwaokoa watoto hawa kutoka kwenye mazingira hayo magumu, kushikamana kwetu tunaweza kuwalisha,kuwavisha, kuwatibu na kuwaelimisha watoto hawa na hivyo tutaweza kujenga taifa bora la kesho.
Imeandikwa na Denis M Nguno
No comments:
Post a Comment