Breaking News
recent

SIMULIZI FUPI: GRACE WA MWANZA

PICHA MTANDAONI
Sura yake iliyokuwa imepauka, nywele zake ndefu zilizokosa
matunzo na midomo iliyokauka sana haikuweza kuificha
historia ya sura yake jinsi ilivyokuwa ikivutia miaka minne
nyuma.
Alikuwa amejikunyata mitaa ya Kariakoo, mbele yake pakiwa
na sufuria dogo. Ndani yake pakiwa na matawi ya mchicha,
yakiwa yamejinyaukia katika namna ya kutia kinyaa. Bila
shaka hata yeye hakupendezwa kuyatazama majani yale.
Haikuwa mara ya kwanza kumuona binti Yule akiwa eneo
lilelile na katika hali ileile ya majonzi.
Ama kwa hakika alikuwa anasikitisha!
Sijui ni kitu gani kiliniaminisha kuwa anaweza kuzungumza
nami walau kwa dakika tano. Kwa sababu niliamini kuwa
hanitambui tena!!
Nikamkaribia na kuulizia bei ya matawi yale ya mchicha.
Alibabaika katika kunijibu na kisha akanitajia bei ambayo
niliamini hata yeye alitamka ilimradi aipate ile pesa.
Nikatoa kiasi cha pesa aliyoihitaji lakini sikuishia kumpatia tu.
Badala yake nilimvuta kando na kisha nikauvunja ukimya.
Nikamweleza kuwa haikuwa mara ya kwanza kuonana naye,
na kidogo ningependa kuzungumza naye.   #djkibara
Akanitazama kabla ya kutoa tabasamu hafifu sana.
Sikuendelea kumtazama machoni badala yake niliinama na
hapo nikaiona miguu yake ilivyopauka na pia akiwa amevalia
kandambili zenye rangi tofauti.
“Ni kipi unahitaji kujua kutoka kwangu ewe mwanaume!”
aliniuliza huku akipepesa macho huku na kule.
Kabla sijasema lolote akajitambulisha kwa jina lake.
“Naitwa Grace wa mwanza… sijui iwapo unalo jingine”
akataka kuondoka nikamdaka mkono, huku nikimkumbushga
kuwa kuwa bado sijampatia pesa yake.
Akanyoosha mkono ili nimpatie pesa lakini badala ya kumpa
pesa nikamwita kwa jina ambalo kamwe hakulitegemea.
“Mwamvita! Nini kilikusibu” nikamuuliza.
Macho yalimtoka, akanitazama mara mbilimbili asipate
kunikumbuka. Nilipoligundua hilo nikajitambulisha jina langu.
Akanisogelea na kisha kunikumbatia kwa nguvu sana, na
hapo nikahisi majimaji ya joto yakipenya katika mwili wangu.
Bila shaka alikuwa analia!
Sikutaka umati utushangae, nikamsogeza Yule binti kando,
tukaufikia mgahawa Fulani usiokuwa na watu wengi. Akaketi
mkabala na kiti nilichokuwa nimekaa mimi.
Hata kabla sijaanza kuzungumza lolote. Huku akiwa
anatokwa machozi Grace wa Mwanza akaanza kunielezea
jambo ambalo lilimfanya awe vile ninavyomuona wakati huu.
“Jimmy, naujutia usichana. Usichana ambao kamwe
hautarejea kamwe, najutia kiburi changu na huu ule urembo
ulionizuzua. Najutia hata marafiki niliowachagua, walikuwa
marafiki wabaya sana. Walinitafutia wanaume na nilitumika
mimi lakini pesa tulitumia pamoja nao. Ama!! Nilikuwa
bwege.
Wakanieleza kuwa mimi ni mrembo na sina hadhi ya kuishi
mjini Mwanza, maneno yao yale ya kipuuzi yakaniingia
kichwani. Hatimaye wakaniunganisha na mwanaume ambaye
aliniahidi kuwa ananileta jijini Dar es salaam kwa madhumuni
mawili. Kunitafutia kazi na kisha kunioa kabisa niwe mkewe
wa ndoa.
Jimmy, mama yangu alinikanya huku analia. Alinisihi sana
nisiondoke Mwanza. Nikamuigizia kuwa nimemuelewa
akapata amani ya moyo, lakini haikuwa vile. Nikaondoka
Mwanza huku nikijisemea kuwa kama yeye mama aliolewa na
baba yangu basi name ni haki yangu kuolewa.
Jimmy, haikuwa ndoa wala haikuwa kazi. Ama kwa hakika Dar
es salaam sio tu ni mkoa wa kipekee bali ni nchi ndani ya nchi
ya Tanzania.
Nchi hii inaweza kukufanya uwe mwehu ghafla na usipate
hata mtu mmoja wa kukushangaa.
Jimmy! Yule kaka aliyejifanya mume mtarajiwa alinitelekeza
kama utani vile baada ya kumgomea aliniponitaka nijiunge
katika danguro na kuuza mwili wangu.
Kutelekezwa huko ukawa mwanzo wa kujiuza bila hiari,
nimetumika Jimmy. Nimetumika sana. Hii ni laana Jimmy.
Laana kutoka kwa mama ambaye nilisikia kuwa aliugua sana
na sikurejea kumuuguza mama yangu.
Nimeteseka hadi hatua hii unionayo, sina thamani hata ya
kukaa ndani ya hoteli hii. Mimi ni mchafu, na sijui kama
sijaathirika. Nahisi mimi si mzima.
Hilo halinishtui lakini Jimmy huenda ni Mungu amekuleta
ukutane nami leo, nakusihi Jimmy. Nichukue Jimmy, najua
haiwezi kuwa kimapenzi kama ulivyohitaji wakati ule lakini
nichukue kama mwanadamu tu anayejutia kila jambo
alilolifanya.
Nichukue unirejeshe nyumbani…. Nimeteseka Jimmy
imetosha!!
Nirejeshe Mwanza Jimmy, nikateseke na kufia huko. Naomba
usiniache Jimmy. Wananibaka kila siku…. Wananitukana kila
kukicha… sina amani hata chembe… sitaki kufia katika nchi
hii iliyo ndani ya nchi. Nchi isiyotambua nini maana ya utu,
nchi inayothamini pesa kuliko kitu chochote, nchi ambayo
ukabila hakuna lakini undugu pia haujulikani.
Nitoe katika nchi hii Jimmy.. nirejeshe nyumbani”
Alishindwa kuendelea kuzungumza Grace wa Mwanza.
Akanifuata nilipokuwa, akapiga magoti na kuendelea kusihi.
Nilijikaza nisitokwe na tone la chozi lakini haikuwezekana,
nikatokwa machozi. Nikamyanyua na kuabiri bajaji
ikatupeleka hoteli niliyokuwa nimefikia.
Nikapanga safari ya upesi upesi.
Siku iliyofuata tukaondoka na Grace wa Mwanza… njia nzima
alikuwa amechangamka sana. Alikuwa anazungumza sana
huku mara kwa mara akijiuliza ni kwa namna gani ataulilia
msamaha kutoka kwa mama yake.
Baadaye alisinzia! Na huo nd’o wakati ambao niliutumia
kutafakari. Niliumia sana kwa sababu Grace hakuwa anaujua
ukweli.
Hakujua kuwa yule mama aliyesikia kuwa aliugua basi aliaga
dunia kwa ugonjwa uleule.
Nilihofia kumweleza maana ningeikatili furaha yake. Na
huenda lingeweza kuzuka tatizo jingine.
Tulifika Mwanza usiku sana, nikachukua vyumba viwili.
Tukapumzika na asubuhi nikamwongoza Grace hadi pale
palipoitwa nyumbani kwao.
Hapakuwa na nyumba bali gofu. Mimi sikuwa jasiri wa
kumueleza nini kilichotokea. Bali majirani tuliowakuta pale
ndio waliomuweka chini na kuzungumza naye.
Naam! Siku nne baadaye mwili wako ulikutwa ukiwa
unaning’inia porini. Watu waliofika wa kwanza eno la tukio
walibahatika kuuona ujumbe uliouacha.
“Sina mama, sina baba, sina rafiki wa dhati bali nina rafiki
mmoja tu mbaya…nina UKIMWI… Siwezi kuishi na rafiki huyu
mbaya.
Wanizike watu wema!!
JIFUNZE: Wazazi ni nguzo muhimu. Tafadhali wasikilize,
waelewe wasemacho. Wana kitu cha ziada ambacho, hata
ufanye vipi hauwezi kuwa nacho.
MWISHO

No comments:

Powered by Blogger.